Swali kwa Mkenya

Kilio ki hapa leo, kilio ki pale na huko kesho,
Kenya mejawa kilio, tutalia hadi mwisho?
Hakina dawa kilio,pasi mtanabahisho,
lipi tumetenda Mola, hasira zitufikie?

Mlipuko hapa leo, mlipuko pale kesho,
Milipuko kila njeo, maisha yafika mwisho,
Wakenya fukara leo, wa ‘hai ufukarisho,
Lipi tumetenda Mola, hasira zitufikie?

Jukumu letu wakenya, vilivyo kujichunguza,
Tupande amani Kenya, amani kuitukuza,
Vitendo vyenye kusinya, tujikaze kupunguza,
Lipi tumetenda Mola,hasira zitufikie?

Kosa ni letu wakenya, upendo tumepunguza?
Kati yetu kapenya, mbawa amani kakimbiza,
Uchangamano wakenya, kamwe tena sipunguze,
Lipi tumetenda Mola, hasira zitufikie?

Kosa ni la viongozi, meshindwa kuunganisha?
Meshindwa na ulinzi, ama vihela kaisha?
Suala la ulinzi, ‘lahitaji mzaha kuisha,
Lipi tumetenda Mola, hasira zitufikie?

Kosa ni la madhabahu, ‘kosa ‘hubiri amani,
Muombeni Mola muhu, wa kuhubiri amani,
Mwombeni ‘tupe suluhu, Kenya ipate amani,
Lipi tumetenda Mola, hasira zitufikie?

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!