Penzi Asili

Yapendeza mapenzi, zaidi ya halwaridi,
Kila uso ni penzi, ‘ngawa halina idadi,
Liuguapo penzi, lanukia ja udi,
Penzi kibisha hodi,hakuna akanushaye.

Akilikosa insi, sijui tumwite nani,
Wasopendana insi, hao ni makauleni,
Kamwe tusiwe wapasi, wala tuwe wapingani,
penzi kibisha hodi, hakuna akanushaye.

Mwenyezi Mungu kaumba, binadamu kwa penzi,
Mbona kuasi Muumba, kwa kukosa penzi,
Mapenzi hutupamba, pambo lenye ulinzi,
Penzi kibisha hodi, hakuna akanushaye.

Kilikanusha penzi, utaishi kwa machozi,
Mapenzi ni ukwezi, kinyume na uumizi,
Tuyalinde mapenzi, tena kwa utunduizi,
Penzi kibisha hodi, hakuna akanushaye.

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!