Kwa Taifa Letu

Kenya taifa letu si, twaienzi sana nchi,
Mungu atupenda sisi, katufanya wananchi,
Ina bora taasisi, za elimu yangu nchi,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Usalama wake nao, ni ule mwema zaidi,
Kachero wema tunao, wa kuchunguza zaidi,
Askari wema tunao, wakamatao ‘ghaidi,
Twaienzi nchi yetu,tuliyopewa na Mola.

Viongozi wema nao, Mungu katuteulia,
Twashiriki wote, nchi nayo yatulia,
Hatuna vurugu nao, ya kuwafanya kulia,
Twaipenda nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Maliasili ni nguzo, msingi wa uchumi wetu,
Pesa kigeni tunazo, ‘leta watalii wetu,
Faranga tulizo nazo, huo ni ukwasi wetu,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Hata bandari tunayo, bandari ya Kilindini,
Na nyingine ijengwayo, i pwani Lamu mjini,
Twaitegemea nayo, itukomboe shidani,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Hata mafuta tunayo, ‘Ngamia 1 Turkana,
Ndiyo tutazamiayo, ‘tukomboe kwa upana,
Maendeleo tunayo, na ajira kwa vijana,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Na chakula tunapata, kamwe hatulali njaa,
Majani chai twapata, mbegu za mahindi pia,
Mapato bora twapata, mashamba yetu yazaa,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

Kiswahili lugha yetu, milele tunaienzi,
Shangwe kwa wazee wetu, milele tutawaenzi,
Ibariki nchi yetu, Ilahi tunaye enzi,
Twaienzi nchi yetu, tuliyopewa na Mola.

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!