Mola Kenya Yakupenda

Ewe Mungu nguvu yetu, twashikuru kwa wemako,
Waipenda nchi yetu, hata nasi wana wako,
Umo mitimani mwetu, wema na fadhila zako,
Nchi yangu yakupenda, uliye Muumba wetu.

Sherehe za kitaifa, sisi huanza kwa dua,
Viongozi wa taifa, bungeni wanapokaa,
Itifaki za taifa, haikosekani dua,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Baada ya machafuko, kuona hasira zako,
Katambua ‘wezo wako, inazengea uso wako,
Tuonyeshe njia zako, milele tuwe wanako,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Kabla ya uchaguzi, Uhuru park kakonga,
Pasipo majikwezi, maombi hukuyapinga,
Tulikuomba Mwenyezi,  amani hukutukenga,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Matendo mabaya hasha, mejitoa lawamani,
Toka wote makausha, hadi baya tamaduni,
Neno ‘ko twalihuisha, kote hadi mitaani,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Lafunzwa somo la dini, shuleni kote nchini,
Vitoto vyafunzwa dini, kosa ‘li tu taabani,
Tunaiheshimu dini, ‘sijetupwa kaburini,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Viongozi dini wengi, walilinda neno lako,
Madhabahu yamo mengi, ‘tolea dhabihu zako,
Wako wafuasi wengi, wanopiga vita vyako,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Tupatapo matatizo, magotini twaanguka,
Tatambua wako ‘wezo, ‘taifa yote tamaka,
Kenya iwe tangulizo, neno lako litamweka,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu.

Milele tonyeshe pendo, na mwelekeo utupe,
Tuchangamane kwa ‘pendo, tusiishe kama kupe,
Kenya ijae upendo, moyo wa pendo utupe,
Nchi yangu yakupenda, uliyemuumba wetu

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!