Shujaa Mstahiki

Kachukua mamlaka, huku mguu kilema,
Mataifa yakamaka, lakini halikulema,
Tukaziomba baraka, sana dhidi ya hujuma,
Kibaki ni mtawala, wa ajabu tena sana.

Kisomo sasa ni bure, wazazi mepumzishwa,
Sijekuwa wanakware, vijana wameridhishwa,
‘ta kama ‘kuna bwerere, maisha merahisishwa,
Kibaki ni mtawala, wa ajabu tena sana.

‘ungana na mataifa, ajili ya biashara,
Na uchumi wa taifa, hapatikani hasara,
Milele njema kaifa, habari za biashara,
Kibaki ni mtawala, wa ajabu tena sana.

Maendeleo dhahiri, kila mja yuwaona,
Bila kutaja twakiri, tunaridhika na kupona,
Sifa njema twahubiri, zake Kibaki jagina,
Kibaki ni mtawala, wa ajabu tena sana.

Watokuwa watawala, Uhuru na wenzako,
Msifanye unyemela, kufanya mengi mauko,
Wacha wenu utawala, umoja uwe mpiko,
Kibaki ni mtawala, wa ajabu tena sana.

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!