Hisia Zangu Halali

Yangu mahututi hali, nimelazwa nakuwaza,
Sinao wingi wa mali, Mola atakuliwaza,
Ndugu hawajatujali , mwachie Mola muweza,
Si la siri hawalali, kutubaidi huweza.

Fikira moyoni mwangu, kwako ziwe mualimu,
Maovu ya ulimwengu, sikubadili  dawamu,
Nimeyaondoa kwangu, moyoni yale awamu,
Sikiza banati wangu, kwako nina kubwa hamu.

Njeri n’onee huruma, siji nikaachilia.
Mola ni mwenye rehema, hali umenijulia,
Mola mejawa huruma,  kifo sitochungulia,
Umewasili mapema, haya tukayangalia.

Ninayo mengi maswali, sidhani una majibu,
Kwa yangu ilivyo hali, usipatwe na aibu
Najua nastahili, ya Mola kali adhabu
Kweli nina mbaya hali, naamini u tabibu.

Siku ikiwa ni njema, huonekana mapema,
Muwi huja kuwa mwema, kale babu alivyosema,
Yakumbuke yangu mema, kama siku ya kiyama,
Puuza mabaya hima, zingatia wangu wema.

Ninalo jambo jingine, tafakari kisikiya
Nilikwona na mwengine, ghere nikamuoneya,
Ukiolewa kwingine, kwangu takuwa hatiya,
Nipe nafasi nyingine, penzi nitakupatiya.

​© Maja Waithaka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!