Nadharia 

Naitunga tungo hini, kuyeleza nadharia,
Kwa waja wa duniani, wafuatao dunia,
Nia zao kutwa duni, dunia ni duni nia,
Ukifuata dunia, niayo itawa duni.

Waishio aushini, aushi itaweshia,
Maisha ni ukingoni, siku wakikufukia,
Uishipi maishani, jua yataisha pia,
Ni mambo yanayoisha, maisha haya sikia.

Mliopo mahabani, naja nanyi kuwajia,
Niwaeleze yakini, ndani ilofichamia,
Mna uhaba hubani, mahaba ninakwambia,
Ni uhaba wa ukweli,mapenzini basi jua.

Waloko uongozini, kututawala raia,
Wamevaa ngozi ndani, uongo kutwongopea,
Daima tubaki chini, wao wanajipandia,
Ya uongo ngozi hini, uongozi fikiria.

Hatima ni ukingoni, kipeo nimefikia,
Mtu upo utu ndani, ndo awe mtu sawia,
Aso utu mtu gani, kiatu kukanyagia!
Mwenye utu insani, huambwa ametimia.

© Bin Mwaguni Rashid

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!