Hupita na Kupituka 

Wasaa ni mpitivu, hupita na kupituka,
Na sekunde huwa pevu, zikageuka dakika,
Mithili yake ni jivu, kwa tufani linofuka,
Au mwangaza mwangavu, umeme yake haraka,
Hupita na kupituka.

Hubadili kuwa kovu, kidonda kilopashika,
Embe biti huwa bivu, wakaa hubadilika,
Wala mwia si mvivu, kweneda kwamba tachoka,
Sultani mwenye nguvu, haungoji angataka,
Hupita na kupituka.

Mwida una ugagavu, kwa ulivyochangamka,
Hujamlisha na mbivu, juani aliyesaka,
Kisha una usongevu, miongo kutoka nyaka,
Katu hauna utuvu, wende ukipumzika,
Hupita na kupituka.

Huchachusha nyama ndavu, nzima ikaharibika,
Ivunde imee kuvu, ioze na kutupika,
Kwa mwia sasa chijomvu, ni kichache chasikika,
Kweli muda ni mwerevu, busara ya kupevuka,
Hupita na kupituka.

Muda sio msikivu, uuite kuitika,
Hutufanya wapumbavu, kutufunza kujuzika,
Kwani huzua maovu, wengi tukakengeuka.
Mendeleo endelevu, kudinda kutofanyika,
Hupita na kupituka.

Ni wangu utamativu, ukingoni nimefika,
Sasa nahisi uchovu, nimechoka kuandika,
Taswira mwia ni shavu, la ajuza kukobweka,
Zifanyie uwekevu, jira nazo huzeeka,
Hupita na kupituka.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!