Si Sukari na Maziwa

Mahaba yana uluwa, wawili wapendanao,
Ikhlasi na takuwa, husonga baina yao,
Hupoa mwenye ku’gua, afua na furahio,
Ni sukari na maziwa. ladhaye mtu kupendwa.

Ni sukari na maziwa, ladha ya huba iwao,
Kopa nzuri kama njiwa, kwa fahari warukao,
Aso wa huba mwingiwa, apatepi raha hio?
Ni sukari na maziwa, ladhaye mtu kupendwa.

Hufanya mtu kulewa, kwa wanywaji wayanywao,
Ukawambaa ukiwa, kubaki nalo pumbao,
Inge’wa kuzawadiwa, ni hidaya ifaao,
Ni sukari na maziwa, ladha ya mtu kupendwa.

Yakini huba ni dawa, hupoa wauguwao,
Nafusi zao huchuwa, kusahau shida zao,
Huba zuri waambiwa, huleta mwema uzao,
Ni sukari na maziwa, ladha ya mtu kupendwa.

Kama sahani na kawa, mahaba wahibanao,
Kwauniana ikiwa, kuna baa kati yao,
Mambo kwao huwa sawa, taratibu bila mbio,
Ni sukari na maziwa, ladha ya mtu kupendwa.

Humshukuru Afuwa, na kila kidogo chao,
Kikubwa ni majaliwa, shukrani ndio zao,
Hawajipi kughuriwa, uchochole wawe nao,
Ni sukari na maziwa, ladha ya mtu kupendwa.

Wavikosapo viliwa, hushukuru tuu wao,
Ni siku mbili zingawa, zinanjaa tumbo zao,
Na bado pamoja huwa, hawawi watenganao,
Ni sukari na maziwa, ladha ya mtu kupendwa.

© Bin Mwaguni Rashid.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!