Juto

Nalitaja lile juto, lonichosha kunichusha,
Kwa vile ving’irimoto, uzushi vilivyozusha,
Tulipokula msoto, shida zikatukausha,
Tukalia sana.

Wakaja watu wazito, wakatupa mshawasha,
Lugha zao za mnato, kwenda kutuwakilisha,
Lile la shida vukuto, wakasema litaisha,
Na tukaungana.

Tuliitikia wito, vyeoni tukawapisha,
Kwa sera zao mseto, ziloahidi bashasha,
Kumbe mafuta ya uto, mwili twaumwagilisha,
Wakaja tukana.

Hata na wetu watoto, wakashindwa kufundisha,
Uchumi ukawa moto, yakagumika maisha,
Fanaka ikawa ndoto, hawakuikamilisha,
Ili kutubana.

Ikawa kama ufito, mwilini kuuchapisha,
Kung’ang’ania mapato, mali wao kujilisha,
Wakasahau vidato, juu viliwapandisha.
Hawakutuona.

Walitufanya mapito, ya wao kujipitisha,
Wafike kuliko vito, wapate jinufaisha,
Mkata kapigwa ngoto, uchungu unaniwasha.
Lini nitapona?

Ni mizigo ya kokoto, ndiyo walitubebesha,
Au kwa lugha mkato, baa walilizidisha,
Kwa kichapo cha kikoto, walichotutembezesha,
Kutokea jana.

Ninaita wangu wito, dhuluma hii kuisha,
Hili la usafi joto, tupate kulisafisha,
Nanga nimeishushato, ujumbe nimeshukisha,
Hivyo buriana.

Bin Mwaguni Rashid.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!