Penda

Penda upendapo pendo, pendo lenye ikrima,
Ikrima njema nyendo, nyendo hishima hikima,
Hikima hata zitendo, zitendo vya kiadhama,
Kiadhama kwa mitindo, kwa mitindo ilo wima,
Kwa mitindo ilo wima,

Wima utovu kando, kando utovu sukuma,
Sukuma lama kwa kondo, kondo upate salama,
Salama uwe muundo, muundo pendo rehema.
Rehema kwani ni nyundo, nyundo kugonga neema.
Nyundo kugonga neema.

Neema na uzalendo, uzalendo nti nzima,
Nzima tufungue fundo, fundo chuki na dhuluma,
Dhuluma liwe ni windo, windo sote kulifuma,
Kulifuma kwa kishindo, kwa kishindo lije koma.
Kwa kishindo lije koma.

Koma na ya mwisho tindo, tindo mwisho ni hatima,
Hatima ya lote rundo, rundo dhuluma kukoma,
Kukoma kwani uvundo, uvundo ndio ujima,
Ujima una magando, magando yanayouma,
Magando yanayouma.

© Bin Mwaguni Rashid

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!