Tungo

Watunzi hutunga tungo, tungo zilizorembeka,
Za muwala na mpango, vina vikatiririka,
Tungo zisizo majongo, mizani ilopangika,
Umeamua ushaha, wazachiani arudhi?

Tungo zisi na maringo, kisha zilonakshika,
Zinasazo kila bongo, zikavutwa kuvutika,
Zikadumu ja mpingo, ja tungo zake Muyaka.
Umeamua ushaha, wazachiani arudhi?

Zimwaye kwenye ulingo, tupate taanisika,
Tungo zisizo na nongo, tungo zilosanifika,
Zilosanwa mviringo, arudhi kuzizunguka,
Umeamua ushaha, wazachiani arudhi.

Tungo zambae uongo, hadaa kuzitamka,
Tungo laini sifongo, kwa zinavyoeleweka,
Tungo zitoe matongo, kwa hadhira kulimka,
Umeamua ushaha, wazachiani arudhi?

Natia nanga ukingo, ngalawa naisimika,
Watunzi Kenya na Bongo, jumuia Afrika,
Tungo mtungapo tungo, arudhi ziwe zashika,
Umeamua ushaha, wazachiani arudhi?

© Rashid Bin Mwaguni.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!