Ukubwa

Nam!Ukubwa jalala, litupwalo kila ozo,
Uozo kila madhila, migogoro na mizozo,
Japo ni hadhi ki mila, ukubwa ni matatizo,
Matatizo na mizozo, ukubwa ndivyo ulivyo.

Mizozo mengi maswala, yalo na vingi vigezo,
Isotaka bongolala, bali fikira mawazo,
Ai!Ukubwa ni ghala, la maneno na mapizo,
Mawazo na maapizo, ukubwa ndivyo ulivyo.

Maapizo na hewala, hupewa kwa muongozo,
Hutaka mja fadhila, kuutoa mwelekezo,
Aah!Ukubwa ni jela, mbona una shinikizo!
Shinikizo Mwwelekezo, ukubwa ndivyo ulivyo.

Shinikizo kutolala, kimoja hata kilazo,
Maozi kuchwa waola, ubunifu bunilizo,
Lo!Utashindwa kula, kwa tabu uletewazo,
Bunilizo ziletwazo, ukubwa ndivyo ulivyo.

Ziletwazo kwa mihula, matukano na mabezo,
Hata watu majuhula, wa fahamu wasinazo,
Ufatwe kila pahala, kwa kauli unenazo,
Unenazo wasinazo, ukubwa ndivyo ulivyo.

Utashangaa salala!tayooneshwa matwezo,
Kutenga lila na fila, huo ndo yako matezo,
Kuamua kwa muwala, taratibu kila wazo,
Matezo na kila wazo, ndivyo ukubwa ulivyo,

Usiwe maziwa lala, ukubwa una uwezo,
Haki ifanye sabila, ujuze waja majuzo,
Sabaa namalizila, Ukubwa haki ni nguzo.

© Bin Mwaguni Rashid.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!