Haki

Haki ninakuandama, ila haki hunitaki,
Wawataka wahashama, pekee wakumiliki,
Haki pindipo u mwema, Iweje kwangu hufiki?
Hunitaki mbona haki?

Wakuhitaji mtima, na haki hukumbatiki,
Wakimbia mayatima, dhulma kwao lukuki,
Haki basi njoo hima, Kwani haki huoneki?
Hunitaki mbona haki?

Iwapo kwa waadhama, waenda telki delki,
Na kwangu mie mjima, kama umejenga chuki,
Haki huji akakoma, huyu dhuluma hatoki?
Hunitaki mbona haki?

Haki japo darahima, ni kwangu hazishikiki,
Haki hata nikisema, sauti haisikiki,
Haki sioni salama, unyoshwe mbona hunyoki?
Hunitaki mbona haki?

Haki haki ima wima, haki wacha kujinaki,
Haki ima wa faima, ninawe sikuepuki,
Haki nimeshika tama, huji kunipiga jeki?
Hunitaki mbona haki?

Haki u kwao daima, na wala kwangu hushuki,
Haki iwe nalalama, husumbuki hushtuki,
Haki umewagandama, hwambiki husemezeki?
Hunitaki mbona haki?

Haki kwa yangu hatima, fata kila mahuluki,
Haki sasa rudi nyuma, sende mbele hakwendeki,
Haki haki Kaditama, dhuluma hahitajiki,
Hunitaki mbona haki?

© Rashid Mwaguni.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!