Lala

Lala ulale salama, lala Milly maridhia,
Lala nitakuandama, uendapo kila ndia,
Lala naja pia mama, naja huko mimi pia,
Na mie nikisinzia.

Lala sina la kusema, isipokuwa kulia,
Lala aona Rahima, lala atakulipia,
Lala mtima wauma, sijiwezi naumia,
Na mie nikisinzia.

Lala nabaki mjima, sina wa kunitania,
Lala raha imekoma, kipi cha kufurahia,
Lala na wako mtima, nipo nakufikiria,
Na mie nikisinzia.

Lala ni yao nakama, hiyo walokufanyia,
Lala dua za karama, mwenza ninakuombea,
Lala lako kila jema, Mola takuwafikia,
Na mie nikisinzia.

Lala chozi nalitema, chozi lajidondokea,
Lala naona huruma, kifua chalowania,
Lala Mola kakutuma, weye alikuchagua,
Na mie nikisinzia.

Lala na yao hujuma, japo walikutendea,
Lala huo ni unyama, naye Rabbi anajua,
Lala mwenzi nna homa, kwamba ulinikimbia,
Na mie nikisinzia.

Lala ila si daima, na mie nitakujia,
Lala lala kaditama, nakuombea Jalia,
Lala nenda kwa Karima, peponi atakutia,
Na mie nikisinzia.

©Rashid Mwaguni.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!