Hunambii Basi

Hunambi mbasi, yayo yaliyokufika,
Vije ujikisi, kalamu ishavunjika,
Una wasiwasi, kwa wino kutawanyika!
Hunambii basi, Kwamba hujui kwandika?

Mwia ni mapisi, hupita na kupituka,
Huku nna ngisi, ana wino nikitaka,
Sitese nafusi, ukaishi kuteseka,
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?.

Tunza ikhlasi, mwenzi isijekutoka,
Kwa maana sisi, waja tunabadilika,
Katu si rakhisi, ya jahara kufichika,
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?

Mekosa fulusi, kununua nachotaka,
Waona taasi , kinena ukisikika,
Kumbe u mweusi, weupe wenda jivika!
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?

Ubure tausi, lorembwa ukarembeka,
Mie wanighasi, Kujinaki usofika,
Kwa sifa sisisi, wasifu usiku mwaka,
hunambii basi, kwamba hujui kwandika.?

Mbona wajibosi, u mkembe hujafika!
Ulete mikosi, kutuka yasiyo tuka?
Lini firigisi, kuwa mwilini mwa nyoka?
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?

Sungura si fisi, tungue meerevuka,
Nawe havipasi, kulia kumbe wacheka,
Si sifa ya nasi, kufanya wakigutuka,
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?

Nami nna hisi, kung’amua yalo shaka,
Najua wa kasi, mtimbifu kitimbika,
Koroto si lasi, ulimwengu ukisuka,
Hunambii basi , kwamba hujui kwandika.

Kwetu sie insi, twenda nyendo kwa mipaka,
Na watunzi nasi, ukingoni tunapaka,
Mwenza linihasi, kutaka usoyataka,
Hunambii basi, kwamba hujui kwandika?

© Rashid Mwaguni Mgute

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!