Ugaidi Tupingeni

Machozi yatumwaika, kucha twazika wendani,
Roho zetu zatutoka, twaishia kaburini,
Machozi yatudondoka, maafa hadi vyuoni.
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Nyoyo zetu zachomeka, kwa uchungu na huzuni,
Ni risasi zapasuka, kila pahali nchini,
Ni juzi yalifanyika, Garissa Mpeketoni.
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Sote tukijumuika, kuidumisha amani,
Utaisha kwa hakika, ugaidi taifani,
Tujue ‘lotuzunguka, tumfahamu ni nani,
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Yapaswa kuhamasika, vijana tujichungeni,
Ugaidi kuepuka, kutongia makundini,
Pamoja kuwajibika, na mbali tuutupeni,
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Tukitaka kuepuka, maafa vitongojini,
Ni umoja kuushika, polisi na insani,
Ugaidi tutazika, na mbali kuutupeni.
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Hali itaimarika, Kenya iwe na amani,
Sote tukishughulika, nyumba kumi vijijini,
Tupatiliapo shaka, turipoti vituoni,
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

Tamati tumeshafika, ughani wetu mwishoni,
Yapaswa kuunganika, Ugaidi tupingeni,
Tutaisha kuondoka, tusipotia manani,
Ugaidi tupingeni, tuidumishe amani.

© Rashid Mwaguni Mgute, 04/6/15

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!