Ya Tatu Unaijua

Oa, ndoa kwa wanopendana, funga pingu za maisha,
Oa,yaani fanana, viwili kifananisha,
Oa,ya tatu mi ndio sina, ndugu yangu nijulisha.

Ua,uzima uwe hakuna, ruhu kuimautisha,
Ua,mfano la asmina, rihi linalonukisha,
Ua,ya tatu ni ipi bwana? ndugu yangu nijulisha.

Tosa,kilo upevu hakina, mdomo kinochachusha,
Tosa,kungia ndani kwa kina, majini kujizamisha,
Tosa,ya tatu katu hakuna, kama iko nijulisha.

Baa,walevi napokutana, vileo kujilewesha,
Baa,ni tatizo kubwa sana, lilo gumu kutatusha,
Baa,ya tatu sijui mbona! kijua nifahamisha.

Kanda,ni video ya kufana, picha inayoonyesha,
Kanda,mahuluki hukandana, viungo kuvinyoosha,
Kanda, ya tatu sijui tena, kikumbuka nikumbusha.

Jua,yani fahamu maana, neno navyomaanisha,
Jua,liangazalo mtana, vitu linalochomesha,
Jua,ya tatu siwezi kana, sijui ibainisha.

Sina,ni mtu anapoguna, kilio kukisitisha,
Sina,sina cha kufanya tena, hatima nnimefikisha,
Sina,tatu haina maana, hata kiilazimisha.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!