Mtoto Mzuri 

Kwangu wewe u johari, furaha wanipatia.
Mwana mtoto mzuri, si kwa umbo si tabia.
Hupaki wala podari, na bado unavutia.
Ngozi laini hariri, pamba inaigizia.
Mwana mtoto mzuri, nakuhibu sana jua.

Jasho lako ni uturi, jinsi linavyonukia.
Kwako hakuna kiburi, nidhamu umejazia.
Kidari chako kadiri, vyema kimesimamia.
Namo mwa wangu suduri, ndo maana ukangia.
Mwana mtoto mzuri, nakuhibu sana jua,

Ninakupenda nakiri, peke ndani ya dunia,
Hisia zinanighuri, nashindwa kuvumilia.
kufu yangu tadubiri, wewe nimekuchagua.
Ndiwe wa moyo sukari, yani wangu maridhia.
Mwana mtoto mzuri, nakuhibu sana jua,

Dira imeshakadiri, moyo ukapenda pia.
Huna hata taksiri, yakini umetimia.
Kwako sina uhodari, mwengine sijajonea.
Si mtunzi mashairi, leo nimekutungia.
Mwana mtoto mzuri, nakuhibu maridhia,

Kisa ni yako athari, kutwa ninakuwazia.
Lini siku itajiri, tukutane maridhia,
Kutwa ninalikariri, jina lako kila ndia,
Kila hali u mzuri, Wallahi wanivutia,
Ninakuaga kwaheri, uwe chini ya Jalia.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!