Yu Wapi? 

Yuwapi mwenye mapenzi, kupoza wangu suduri?
Ambaye atanienzi , kwa mahaba tadubiri,
Afute zangu simanzi, za mwanzo zilizojiri,
Haya basi nionyeshe, mwengine zaidi yako.

Yuwapi huba mjenzi, alo mahaba tajiri,
Mwana asemikunyanzi, bali ngozi ja hariri,
Mwenye mapenzi ya panzi, kwa kunibeba vizuri,
Yuwapi zaidi yako? kama yupo nionyeshe.

Yuwapi msijang’onzi, yani aso na kiburi,
Awe ni wangu kurunzi, kila laili wa nnahari,
Anangazie mionzi, awe ni wangu wa heri,
Kama yupo nionyeshe , mwengine zaidi yako.

Yuwapi aso vitenzi, tamaa isomghuri,
Setaka vya Uholanzi, aishiye bila gari,
Mpenzi wangu utenzi, apendaye ushairi.
Yuwapi unionyeshe, mwengine zaidi yako?

Yuwapi penzi mlinzi, kwa ya moyo wa manowari,
Asiyenipa majonzi, wakunepushia shari,
Mwenye hadhi ya utunzi, apendaye ushairi,
Yuwapi unionyeshe, mwengine zaidi yako?

Ni wewe huba mjenzi, njoo ninakusubiri,
Mpenzi wangu utenzi, upendaye ushairi,
Na wala sioni mwenzi, zaidi yako nakiri,
Yuwapi unionyeshe, mwengine zaidi yako.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!