Mbona

Penzi limeniadhibu, kunitonesha kidonda.
Na yote ndiwe sibabu, laazizi kukupenda.
Mie mwenzi nakuhibu, ila mbona wanitenda?
Mbona unaiadhibu, nafsi isiyo na kosa?

Huba umeliharibu, kwenda kulipondaponda.
Ukaja kunipa tabu, kulitupa langu tunda.
Zimewa chungu zabibu, tamuye umeivunda.
Mbona unaiadhibu, nafsi isiyo na kosa?

Ni yepi yalokuswibu, mahaba yakakushinda?
Hadi wako mahabubu, msimamo ukapinda?
Ukaacha utabibu, ukaniacha nakonda!
Mbona unaiadhibu, nafsi isiyo na kosa.

Mie nilistahabu, kijua utanilinda.
Nikakuita sahibu, sahibu pete na chanda.
Hivi ulonipa jibu, wataka nivisha sanda?
Mbona unaiadhibu, nafsi isiyo na kosa?

Mahabuba lijaribu, kuenzi na kukuganda.
Kumbe ulinighilibu, kusema utanilinda.
Ndio ikawa sababu, nakumbuka mla ganda.
Mbona unaiadhibu , nafsi isiyo na kosa?

Umenipa masaibu, mawazo yamenitanda.
Nilipo sina jawabu, mwili u kama wa ng’onda.
Yote hayo kwa sababu, nakupenda sana nyonda.
Mbona unaiadhibu, isiyo na kosa?

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!