Uwazaji Tunduizi

Waza, ewe uwazae, uwaze kutenda kazi,
Waza, baa utangue, usuluhivu mwenezi,
Waza, jukumu livae, ewe tatizo tatuzi,
Uwazaji tunduizi.

Waza ,wajibu utwae, mawazo mema mwenezi,
Waza, tamuli yandae, mawazo ya kiganguzi,
Waza, uyapambanue,ya nyakanga nyakanguzi,
Uwazaji tunduizi.

Waza, suluhu lipae, ueleze waziwazi,
Waza, ukayagangue ambayo hawayawezi,
Waza, tata utegue, tendawili mteguzi,
Uwazaji tunduizi.

Waza, bongo lisumbue, ndipo uwe mgunduzi,
Waza, zibo uzibue, palozibwa pawe wazi,
Waza, giza,litandue, mwenge ung’ae ja mwezi,
Uwazaji tunduizi.

Waza, nikutamatie, hizi beti tano hizi,
Waza, mengi yakufae, wewe mwenye masikizi,
Waza, kodoa yang’ae, yaole yako maozi,
Uwazaji tunduizi.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!