Mtegaji Mteguzi

Kila wa fumbo mfumba, iye ndiye mfumbuzi.
Na mlumbi hatalumba, asipo’wa na ujuzi.
Mgomba wotao tumba, ndio uzaao ndizi.
Mtegaji mteguzi.

Hawezi kusuka kumba, asoujua mnazi.
Kubwa halitomkumba, asokuwa mtatuzi.
Mganga akijigamba, si ganga ni mganguzi.
Mtegaji mteguzi.

Hata mtambi kutamba, hawi bila utambuzi.
Mpambe kwenda jigamba, huyo jua mpembuzi.
Naye mnoa vigumba, na sibabu ya unozi.
Mtegaji mteguzi.

Huumbui aloumba, Mola Mterehemezi.
Wala haachi kutimba, asokuwa na mbawazi.
Endaye piga marimba, kwa hayo ni mbobezi.
Mtegaji mteguzi.

Kaditama nishagomba, lowa nayo magombezi.
Kodi mlipia chumba, ni yule mtenda kazi.
Kufumbua na kufumba, huwa kwa mwenye maozi.
Mtegaji mteguzi.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!