Rahisi

Rahisi haihahalisi,
rahisi huwa na hasi,
rahisi inafilisi,
sende kuikumbatia.

Rahisi ewe mbasi,
rahisi ina visasi,
rahisi hata matusi,
utatukanwa kulia.

Rahisi ina utesi,
rahisi haitupasi,
rahisi huzua kesi,
segerea kuishia.

Rahisi huua hisi,
rahisi pia yaghasi,
rahisi ina najisi,
mbona waifuatia?

Rahisi ni mahsusi,
rahisi ni ya waasi,
rahisi kwao wakwasi,
ina lengo nakwambia.

Rahisi bila kiasi,
rahisi ina mikosi,
rahisi takukorosi,
kukuchoma kuungua.

Rahisi iwe fulusi,
rahisi na kwetu sisi,
rahisi ina nukhusi,
ni rahisi inaua.

Rahisi ina nakisi,
rahisi siri nakisi,
rahisi sio nyepesi,
ni habta hiyo pia.

Rahisi si ikhilasi,
rahisi sio ya insi,
rahisi mwachie fisi,
vya bure mng’ang’ania.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!