Kipi Kilitangulia

Mizingile wazinguzi, wa mafumbo yalozonga,
Wahenga na wahenguzi, watunzi wajua kunga,
Muujuao ujuzi, kufungua palofunga,
Naziomba kumbukizi, msambe mnanikenga,
Baina kuku na yai, kipi kilitangulia?

Nyakanga na nyakanguzi, watunza kunga nyakanga,
Nipeni jawabu wazi, liso na kuniviringa,
Japo kuku ndo mzazi, yai ndiye alotunga,
Kuku kuwako hawezi, bila yai kujijenga,
Baina kuku na yai, kipi kilitangulia?

Magwiji wa uchunguzi, niondoeni ubunga,
Waganga na waganguzi, wapunga pepo kupunga,
Dadavua dadavuzi, tungo mnaozitunga,
Nipeni wenu wamuzi, wa fahiwa zilokonga,
Baina kuku na yai, kipi kilitangulia?

Nioneeni mbawazi, ya ikrari kugonga,
Msiifanye henezi, jawabu mnapopanga,
Si njema katu ajizi, ajizi inabananga,
Ajizi ni banangizi, hututia za mtonga,
Baina kuku na yai, kipi kilitangulia?

Alo na jibu nyerezi, anijibu kwa kutunga,
Na mwenye ufafanuzi, anifunue maninga,
Beti sita tamatizi, mdahalo naufunga,
Hapa naishusha ngazi, kuitia yangu nanga,
Baina kuku na yai, kipi kilitangulia?

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!