Mapenzi

Mapenzi ndumakuwili, yauma yakipuliza,
Mapenzi kama asali, utamuwe kisikiza,
Mapenzi pia shubili, matungu nakueleza.
Yauma yakipuliza.

Mapenzi japo samli, kooni yanakwaruza,
Mapenzi ni makatili, nayo sende jiapiza,
Mapenzi watu wawili, watatu huyakatiza,
Kooni yanakwaruza.

Mapenzi yana thakili, yaepuke ukiweza,
Mapenzi ni idhilali, epuka nakuepuza,
Mapenzi hayana nguli, kila mja yaumiza,
Yaepuke ukiweza.

Mapenzi yepuke mbali, dawama yanaduwaza,
Mapenzi hudhofi mwili, ndwele kukuambukiza,
Mapenzi yepuke mbali, mavani yatakungiza,
Dawama yanaduwaza.

Mapenzi ni ya azali, wengi yaliwatatiza,
Mapenzi tangu asili, ya shaibu na ajuza,
Mapenzi lumbwi sahili, rangi yanajigeuza,
Wengi yaliwatatiza.

Mapenzi nikiyakuli, yanatisha kama kiza,
Mapenzi usikubali, moyoni kuyadekeza,
Mapenzi raha lailai, ni wengi yawakoseza,
Yanatisha kama kiza.

Mapenzi saba kamili, kaditama namaliza,
Mapenzi mara ya pili, chunga mie nakujuza,
Mapenzi ni pilipili, mwasho wake unaliza.
Kaditama namaliza.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!