Mtu na Utu

Mtu hujaitwa mtu, mtu awapo na utu.
Mtu akosapo utu, si mtu ni mtu chatu,
Mtu ni utu si kitu, si kitu mtu ni utu.
Alo mtu msi utu, mtu hayawani mwitu.

Si mtu ni nyamamwitu, mtu auaye mtu,
Mtu kupiga mtutu, mwenziwe haimfutu,
Mtu so’thamini utu, ni mtu roho ya kutu,
Mtu hayawani mwitu, alo mtu msi uti.

Alo mtu msi utu, hajawa ni mtu katu!
Mtu niseme patatu, huyo ana hisi butu,
Mtu alo hisi butu, si mtu bali kiatu,
Alo mtu msi utu, mtu hayawani mtu.

Watu tushikeni utu, ndo kwamba tuitwe watu,
Utu twambate papatu, awali hadi tamatu,
Mtu asoshika utu, ni mtu mwenye majutu,
Mtu hayawani mwitu, alo mtu msi utu.

© Rashid Mwaguni Mgute

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!