Hutanda na Kunyauka

Hata uwapo hawinde, usende kusalitika.
Kusalitika usende, nao ukenda jivika.
Kujivika usipende, maovu yatakufika.
Utajiri ni umande, hutanda na kuyayuka.

Hata na juu upande, kisha jua utashuka.
Nao utamu wa tende, kwa shubili huchunguka.
Ulivyo ni peremende, kimumunywa huishika.
Utajiri ni umande, hutanda na kuyayuka.

Baadeni huja bonde, kila palipoinuka.
Na palipo fufutende, ubaridi hupashika.
Sijikenge uugande, mwisho utakuganduka.
Utajiri ni umande, hutanda na kuyayuka.

Nawambia chondechonde, epukeni ya hakika.
Msije mkala kunde, mashuzi yakaalika.
Tiba ni bora jilinde, kabila hujagonjeka.
Utajiri ni umande , hutanda na kuyayuka.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!