Nimechoka na Utumwa

Naishi maisha, aushi ya sikitiko, yenye dhiki na udhia,
Ya kutamausha, yasoisha taamauko, huzuniko na tanzia,
Kwa kunidunisha, na huo umero wako, kutwa wanifinyilia.
Nimechoka na utumwa!

Umenizoesha, kunipa makombo yako, vichafu kunitupia,
Zimeshanichosha, geresha hizino zako, nawe najitanibia,
Nausimamisha, sitaki msada wako, mwenye tajitegemea,
Nimechoka na utumwa!

Umenihurisha, nitende yangu kwa mbeko,
kwamba ni mja huria, Waniamrisha, kwao vibaraka wako, siwezi jiamulia!
Unanitumisha, mbona huli jasho lako, ukacha kuniibia?
Nimachoka na utumwa!

Umenizindusha, umeshanipa zinduko, nacha kukutumikia,
Umeitorosha, haki kuifanya yako, haki umeichukua,
Ninaiangusha, ikumbwe na poromoko, dhulumayo nakwambia,
Nimechoka na utumwa?

Nari nishawasha, ni ange lau viboko, chapa nitavumilia,
Limeshanitosha, sitaki tena sumbuko, uonevu kuzidia,
Sinayo bashasha, Afrika dhulumiko, kila kukicha nalia,
Nimechoka na utumwa!

Ninahitimisha, mweusi ifate miko, unajikengeukia?
Wacha mshawasha, shika dasturi zako, uwache kuigizia,
Huyo anatisha, fuata ruwaza zako, pia nazo hutimia,
Nimechoka na utumwa!

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!