Kurunzi ya Maisha 

Nilipata afueni, pindi nilipodamka,
Nilipokuwa ndotoni, macho yalinifunguka,
Nikaangaza mbeleni, nikaiona baraka,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Nyanya alinieleza, angalipata nafasi,
Ambayo hangeliweza, kisa ya mila nakisi.
Baraka alinituza, ili niweze kupasi,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Ikawa kiguu na njia, kuelekea shuleni,
Niliyaangazia, maisha ya nyumbani,
Tulichokitegemea, hakikutosha asilani,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Ushauri wa mwalimu, kusukuma gurudumu,
Ukaniweka kwa hamu, ya kuchukua jukumu,
Ya kutengeneza utamu, kama ule wa filamu,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Nikabukua vitabu, usiku hadi mchana,
Mitihani nikaijibu, nilichopanda kavuna,
Nikipasi kiajabu,na alama nyingi sana,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Nikajiunga na chuo, kusomea taaluma,
Wasamaria ndio, waliotoa ndarama,
Baada ya vijilio, vya karo kuwaandama,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Baada ya kupata shahada, niliajiriwa kazi,
Kazi niliyoipenda, sababu ya kuwa wazi,
Hili lilikuwa tunda, la bidii yangu ya juzi,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

Baada ya kuliwaza, hilo ndoto la ajabu,
Nimeamua kuanza, kupata elimu tubu,
Kwa hakika nitaweza, kwenda shule ya karibu,
Kurunzi ya maisha, elimu ndiyo maisha.

© Samwel mwangi Gathia

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!